(ABNA24.com) Kuingia madarakani nchini Uingereza Boris Johnson kama Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo kumeibua wasiwasi wa nchi hiyo kujitoa katika Umoja wa Ulaya bila kufikiwa mapatano, jambo ambalo litakuwa na matokeo mabaya sana ya kiuchumi na kiusalama kwa nchi hiyo.
Katika msimamo wake mpya alioutangaza Jumamosi tarehe 27 Julai, Johnson amewaonya wanachama wa Umoja wa Ulaya kwamba iwapo wataendelea kusisitiza kuwekwa vizuizi au vituo vya mpakani na Ireland, basi Uingereza itajitoa katika umoja huo kupitia Brexit ngumu au bila ya kufikiwa mapatano na umoja huo. Hali ya utata ya mpaka wa Ireland Kaskazini na Jamhuri ya Ireland (Ireland Kusini) baada ya Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya ni suala gumu zaidi kuhusiana na kadhia nzima ya Brexit. Hivi sasa hakuna kituo chochote cha mpakani kilichopo kati ya Ireland Kaskazini na Jamhuri ya Ireland wala shughuli zozote za forodha zinazofanyika kati ya maeneo hayo.
Takwa la Johnson kwa sasa ni kuwa baada ya Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya, Brexit, hali ya maeneo mawili hayo iendelee kubakia kama ilivyo hivi sasa, lakini Umoja wa Ulaya unapinga jambo hilo na kutaka vizuizi vya mpakani viwekwe kati ya Ireland Kaskazini na Jamhuri ya Ireland. Johnson anataka mazungumzo mapya yafanyike kati ya pande mbili na kufutiliwa mbali kipengee kinachotaka kuwekwa vizuizi katika mipaka ya maneo hayo katika mazungumzo ya Brexit.
Katika kutaka kujua iwapo kuondolewa vizuizi kati ya mpaka wa Ireland Kaskazini na Jamhuri ya Ireland ndilo takwa lake la pekee, Johnson ameibu kwa kusema: Iwapo tutaondoa kabisa vizuizi hivi na kwa namna ya kudumu, tutakuwa tumefikia maendeleo makubwa.
Mwezi Januari mwaka huu, wabunge wa Uingereza walipinga kwa sauti moja kipengee kinachohusiana na nchi hiyo kujitoa katika Umoja wa Ulaya kwa sharti la kuwekwa vizuizi hivyo vya mpakani. Theresa May, Waziri Mku wa Uingereza aliyejiuzulu hivi karibuni kutokana na suala hilo la Brexit alifanya mazungumzo ya muda mrefu na Umoja wa Ulaya kuhusiana na suala hilo lakini bila ya mafanikio yoyote.
Kutotatuliwa suala hilo kumeibua wasiwasi mkubwa kati ya viongozi wa Jamhuri ya Ireland. Wanahofu kwamba iwapo vizuizi vya mpakani vitawekwa katika mipaka ya jamhuri hiyo na Ireland Kaskazini, vitabana safari za watu wa Ireland mbili hizo na kuibua machafuko ya Wakatoliki wa Ireland Kaskazini na hivyo kuzua tena vita vya ndani baina ya Wakatoliki wanaotaka mfumo wa Jamhuri na Waprotestanti wanaotaka mfumo wa ufalme.
Akizungumzia suala hilo hivi karibuni, Leo Varadkar, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Ireland amesisitiza kwamba iwapo Uingereza itajitoa katika Umoja wa Ulaya bila kufikia mapatano ya mwisho, suala la kuanza tena mjadala wa kuunganishwa Jamhuri ya Ireland na Ireland ya Kaskazini halitaepukika.
Kwa maelezo mengine ni kwamba Waziri Mkuu huyo anaamini kuwa iwapo Uingereza itajitoa katika Umoja wa Ulaya bila kufikiwa mapatano ya mwisho mjadala wa kuziunganisha Ireland mbili hizo hautaepukika. Matamshi ya Waziri Mkuu huyo yamekabiliwa na radiamali hasi na kali ya chama cha Ireland Kaskazini cha Democratic Unionist Party DUP ambacho ni chama kikubwa zaidi kinachoiunga mkono serikali ya Uingereza. Hivyo, imebainika wazi kuwa mbali na matokeo mabaya ya kiuchumi na kibiashara yatakayosababishwa na kujiondoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya, hali hiyo pia inaweza kuandamana na matokeo hatari ya kiusalama yanayoweza kuibua malalamiko na upinzani mkali katika eneo la Ireland Kaskazini.
Kwa msingi huo, tunaweza kusema kuwa suala la kujitoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya ambalo mwanzoni lilionekana kuwa ni jambo raisi, hivi sasa limebadilika na kuwa changamoto kubwa kwa nchi hiyo, changamoto ambayo inazidi kuwa ngumu siku baada ya nyingine. Ikiwa imepita miaka mitatu tokea kufanyika kura ya maoni ambapo asilimia 52 ya Waingereza waliamua kuitoa nchi yao katika Umoja wa Ulaya (Brexit) na miaka miwili tokea umoja huo ujulishwe rasmi msimamo huo, bado serikali ya Wahafidhina ya London haijafanikiwa kuwaridhisha wananchi wa nchi hiyo kuhusiana na suala hilo. Suala la Brexit limeendelea kuwa tata zaidi na kuibua changamoto za kisiasa, kiusalama na kiuchumi ambazo zimewatia wengi wasiwasi. Suala muhimu hapa ni kwamba Umoja wa Ulaya hauko tayari kubadilisha chochote, likiwemo suala la hali ya mipaka ya Ireland mbili, katika mazungumzo ya Brexit yaliyofikiwa kati ya umoja huo na Theresa May mwezi Novemba mwaka uliopita. Tayari Jean-Claude Juncker, Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya amemwambia Boris Johnson kwamba mapatano ya Brexit hayawezi kubadilishwa.
Msimamo huo wa Brussels umemwachia Waziri Mkuu wa Uingereza machaguo mawili magumu ya ima akubali mapatano ya Brexit kama yalivyo hivi sasa ua ajitoe kwa namna ngumu katika Umoja wa Ulaya.
/129